Press Release (Kiswahili Version)

Hifadhi ya Nyaraka Za Mijadala ya Bunge Kwenye Mtandao: 1960-2011

Kwa ushirikiano na:

  1. Kenya National Assembly
  2. Google Kenya
  3. Kenya ICT Board

 

 

Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria ni nini?

Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria ni nini?

Ni shirika la serikali katika Idara ya Mahakama. Jukumu lake ni kuchapisha Ripoti za Kisheria za Kenya (ambazo ni ripoti rasmi za Kenya za maamuzi ya Mahakama ya Juu Kabisa, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu), kuhakiki na kuchapisha Sheria za Kenya na kuchapisha nyaraka zingine zozote husika.

Nini habari kuu?

Nini habari kuu?

Wakenya sasa wanaweza kupata rekodi za kihistoria na za sasa za mijadala ya Bunge la taifa pamoja na bunge za awali na sheria za tangu 1960 kufikia sasa 2011.

Je, mtu atapata wapi rekodi hizi?

Je, mtu atapata wapi rekodi hizi?

Kwenye tovuti rasmi za taasisi zifuatazo:

Nini kilicho kwenye rekodi hizi?

Nini kilicho kwenye rekodi hizi?

Rekodi hizo ni mijadala ya bunge mbalimbali za Kenya, yaani Baraza la Bunge kabla ya uhuru (linalofahamika kama Leg-Co), Bunge la Wawakilishi la baada ya uhuru na baadaye, Bunge la Kitaifa. Rekodi hizi kirasmi huitwa Hansard.

Hansard ni nini?

Hansard ni nini?

Hansard ni jina la rekodi rasmi za mijadala ya bungeni. Neno hilo linatumika sana na mataifa ya Jumuiya ya Madola ambayo yana mfumo wa bunge unaotoka ama unaofuata mfumo wa Uingereza/Westminster.

Nini umuhimu wa rekodi hizi?

Nini umuhimu wa rekodi hizi?

Rekodi hizo zina habari za thamani kubwa sana kwa urithi wa jamii, kisheria, siasa za Kenya. Kuanzia kwa mijadala ya bunge inayozungumzia mpito hadi serikali ya kujitawala wenyewe mpaka kuzaliwa kwa Jamhuri ya Kenya; kuanzia kutangazwa kwa Mau Mau kuwa chama kisicho halali mnamo 1952 hadi kuondolewa kwa tangazo hilo mnamo 2003. Rekodi hizo ni hazina ya thamani sana ya ufahamu na habari kuhusu utawala wa Kenya. Raia sasa wanaweza kutafuta, kupata na kurejelea kwa urahisi habari muhimu zinazolingana na muktadha, kutoka kwa mijadala ya bunge inayohusu masuala yanayoathiri maeneo bunge yao ama suala ambalo linawahusu kwa njia fulani. Wasomi wa kisheria na maafisa wa mahakama wanaweza kutafiti kwa urahisi muktadha wa kihistoria ambao sheria fulani na sera zilipitishwa na bunge.

Rekodi hizo zimekuwa wapi?

Rekodi hizo zimekuwa wapi?

Rekodi hizi awali zimekuwepo kwa umma kwa njia ya karatasi kama sehemu ya rekodi za umma za Bunge la Kitaifa na Hifadhi ya Kitaifa. Hata hivyo, kwa sababu zilihifadhiwa kama karatasi, ufikiaji wake na umma ulizuiwa. Bunge la Taifa tangu 2007 limekuwa likirekodi vikao vyake kwa njia ya tarakimu na kutoa fursa ya kufikia rekodi hizi kupitia tovuti yake www.parliament.go.ke.

Rekodi hizi zilipatikanaje kwenye tovuti?

Rekodi hizi zilipatikanaje kwenye tovuti?

Rekodi za kabla ya 2007 zilipatikana kwa njia ya karatasi pekee na hivyo hazingeweza kupatikana na kuchambuliwa kwa urahisi. Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria kwa ushirikiano na Bunge la Kitaifa zilibadili rekodi hizi za makaratasi kuwa nyaraka za tarakimu na kisha kutumia teknolojia ya Google ya kuorodhesha na kusaka habari ili kuwapa njia rahisi ya kutafuta na kudurusu rekodi huku zikisalia katika hali yake asili.
Hii ni moja ya juhudi za mradi unaonuia kuimarisha fursa ya raia kufikia habari halali za umma unaohusisha Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria, Bunge la Kitaifa, Bodi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Kenya (Kenya ICT Board) na kampuni ya Google.

Rekodi hizi zimekamilika kwa kiwango kipi?

Rekodi hizi zimekamilika kwa kiwango kipi?

Kufikia wakati wa tangazo hili, toleo la mapema la Hansard zilizokusanywa na kuorodheshwa ni ripoti ya kikao cha nne cha mijadala ya Baraza la Bunge ya tarehe 22 Machi, 1960. Rekodi hivi karibuni pia zinapatikana. Rekodi za hapo awali, yaani rekodi za kabla ya 1960, zitazidi kuchapishwa kwenye kitovu hiki kadiri zinavyobadilishwa kutoka hali ya karatasi kuwa nyaraka za tarakimu.

Na rekodi za wakati huu na za siku zijazo, je zitaendelea kupatikana kupitia kwa kitovu hicho cha tovuti?

Na rekodi za wakati huu na za siku zijazo, je zitaendelea kupatikana kupitia kwa kitovu hicho cha tovuti?

Kitovu hicho kimeundwa ili kutoa habari za kihistoria zilizoko katika Hansard, nyingi ambazo zilitayarishwa na kuhifadhiwa kama makaratasi pekee. Kitovu hicho ni njia spesheli ya kurahisisha kufikia, kuchambua na kurejelea mrundo wa makaratasi yaliyonakiliwa kwa skena. Kwa sababu rekodi za sasa na baadaye zitanakiliwa na kusambazwa kama nyaraka za kompyuta, zaweza kupatikana kwa njia tofauti kwenye tovuti inayotoa hata fursa zaidi ya kudurusu na ufikikaji. Njia hii mpya ya rekodi za sasa ndio Baraza la Kitaifa la Kuropoti Sheria na washirika wake katika mradi huu wanashughulikia. Hata hivyo, hadi mbinu hii itakapoundwa na kuanza kutumika, rekodi za sasa za Hansard zitapatikana kupitia kitovu hicho.

Nini inafanya njia hiyo kwenye tovuti ambapo rekodi hizi zinapatikana spesheli?

Nini inafanya njia hiyo kwenye tovuti ambapo rekodi hizi zinapatikana spesheli?

Ni suluhisho bora la kuweka, kuorodhesha, kuchambua na kudurusu nyaraka, vitabu na majarida. Kupitia teknolojia ya kisasa ya kutwaa habari za vitu, OCR (object character recognition), mambo ya kihistoria yaliyonakiliwa kupitia mashine ya chapa ama njia ya picha sasa yana maandishi yake katika orodha na yanaweza kutafutwa kikamilifu. Hii inawapa wasomaji habari ambazo hawangepata, kwa njia ile ile ya picha ambayo nyaraka zimekuwepo.

Je, rekodi hizi ni sawa kivipi?

Je, rekodi hizi ni sawa kivipi?

Rekodi hizo zimewasilishwa kwa hali halisi kama rekodi asili za makaratasi ambako zilitolewa.

Je, rekodi hizi ni sawa kivipi?

Je, rekodi hizi ni sawa kivipi?

Rekodi hizo zimewasilishwa kwa hali halisi kama rekodi asili za makaratasi ambako zilitolewa.

Je, rekodi hizi zimepewa haki ya kunakili?

Je, rekodi hizi zimepewa haki ya kunakili?

Rekodi ya mijadala ya Bunge ni habari za wazi kwa umma. Huchapishwa na Serikali na kutolewa kwa raia wake bila malipo. Hakuna vizuizi kuhusu utumiaji wa habari hizi.

Je, mtu anaweza kuchukua, kuchapisha na kuhifadhi rekodi hizo?

Je, mtu anaweza kuchukua, kuchapisha na kuhifadhi rekodi hizo?

Sio kwa wakati huu. Hata hivyo, wanaozitumia wanaweza kupata nakala na kusambazia wengine anwani ya kupata rekodi yoyote katika hifadhi au kwa kutumia mbinu ya tarakilishi ya ‘print-screen’, kuchapisha kurasa ya rekodi hizo ambayo imeonyeshwa kwenye uso wa tarakilishi kwa wakati fulani.

Je, mradi huu unagharimu pesa ngapi?

Je, mradi huu unagharimu pesa ngapi?

Gharama pekee za moja kwa moja za mradi huu zilikuwa malipo kwa wataalamu zilizolipwa na Bunge la Kitaifa na Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria, ambazo zilihusu kubadilisha rekodi za makaratasi hadi faili za tarakimu. Gharama hii ilikuwa takriban Kshs 2 milioni. Pamoja na hayo, kila mshirika alitoa ujuzi muhimu wa kiufundi na kikazi, hasa kampuni ya Google iliyoorodhesha rekodi hizo bila malipo na kuunda mbinu hiyo ya kiteknolojia ambayo rekodi zitatafutwa na kusambazwa kwa urahisi kwenye mtandao.


Habari zaidi kuhusu mradi:

Jina la mradi: ‘Open Access to Public Legal Information’

Msingi
Huku sehemu 35 ya Katiba ya Kenya 2010 ikieleza haki ya raia kupata habari za umma, ufikikaji halisi wa habari halali za umma unazuiwa na miongoni mwa mambo mengine njia ambayo habari hii inatolewa. Chanzo, usimamizi na utoaji wa habari halali za umma Kenya (Sheria za Kenya; Maamuzi ya Mahakama; Rekodi za Mijadala ya Bunge; Notisi za Kisheria; Notisi kwenye Gazeti la Serikali; Miswada ya Bunge na Mikataba na Sheria za Kimataifa) haijawekwa katika mfumo mmoja ambao unatoa nafasi kwa raia kupata habari hizo kwa urahisi wakitumia teknolojia za sasa na zinazoibuka.
Ukizingatia taasisi anuwai zinazohusika na suala hili zima la habari halali za umma, kuna haja ya kutumia mbinu inayoweza kugawanywa na kutumiwa na wengi, iliyo wazi, yenye ukwasi wa semantiki na inayotumia teknolojia yoyote ili kuimarisha matumizi tena ya data, ubadilishanaji wa data, kurekodi mzunguko wa kutumia mitambo inayojiendesha na kusanifisha uwasilishaji wa data na metadata. 


Malengo

Kuimarisha uwezo wa Baraza la Kitaifa la Kuriporti Sheria wa kujiweka kama taasisi ya kutazamiwa katika usimamizi na utoaji wa habari halali za kisheria kwa umma;

Kutoa fursa ya kupatikana kwa habari halali za umma bila malipo kupitia mbinu njema ya kutafuta na ya haraka;

Kuunda na kutekeleza utaratibu wazi, unaofanya kazi na usioegemea teknolojia katika usimamizi wa habari halali za umma za sasa na baadaye.

 

Mashirika yanayohusika na majukumu yao

Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria (National Council for Law Reporting)– mwenye kutoa mwaliko kwa wanaoshiriki na anayeongoza utekelezaji;

Bunge la Kitaifa – shirika linalotekeleza na mtoaji habari;

Mchapishaji wa Serikali (Government Press) – shirika linalotekeleza na mtoaji habari;

Bodi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Kenya ICT Board) – usaidizi wa nyenzo kupitia mradi wa kuweka miundo msingi ya uwazi katika mawasiliano, Kenya Transparency Communication Infrastructure Project (TCIP);

Kurugenzi ya Mfumo wa Elektroni wa Serikali, (Directorate of e-Government) – ushauri wa kiufundi kuhusu mbinu na taratibu katika mfumo huu wa e-government;

Mshauri wa kiufundi wa Mpango wa Utekelezaji wa kuunganisha bunge za Afrika kwenye mtandao (i-Parliaments Action Plan), wa Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii Afrika katika shirika la Umoja wa Mataifa (UNDESA), kuhusu uundaji wa utaratibu wazi, wenye ukwasi wa semantiki na unaotumia teknolojia yoyote kuweka rekodi za bunge, sheria na mahakama .

Kampuni ya Google – mshiriki katika teknolojia ya kuorodhesha na kutafuta.


Julai 2011

Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria

Kuhawili Fasihi za Kisheria kuwa Manufaa Kwa Umma

 

Baraza la Kitaifa la Kuripoti Sheria, Kwa Bidii ya:      
Siphira Gatimu · Martin Andago · Lameck Oyare . Michael Mayaka · Nicholas Okemwa · Michael M. Murungi · Musembi Kasavu