You are here:       
Kenya Law / Blog / Presidential Election: Kesi Ya Uchaguzi Wa Kirais: Toleo Jepesi Kwa Mwananchi

Kesi Ya Uchaguzi Wa Kirais: Toleo Jepesi Kwa Mwananchi

To read the Plain language analysis in English, click here.

Uchambuzi huu wa lugha nyepesi umetayarishwa na Baraza la Kitaifa la Kuripoti maswala ya Kisheria (National Council for Law Reporting) kwa uelewa bora zaidi wa umma kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi kwenye kesi ya uchaguzi wa kirais iliyohitimishwa hivi majuzi.

Raila Odinga & wengine 5 v Tume Huru ya Uchaguzi & Mipaka & wengine 3 [2013] eKLR
Mahakama ya Juu zaidi ya Kenya
WM Mutunga CJ & PK Tunoi, MK Ibrahim, JB Ojwang, SC Wanjala, NS Ndungu SCJJ
Machi 30, 2013 & Aprili 16, 2013

Mhariri: Michael M. Murungi. Wanaripota wa Kisheria: Monica Achode, Emma Kinya, Teddy Musiga
Tafsiri: Bw. Mpasua Msonobari

 

Mahakimu wa Mahakama ya Juu Zaidi katika kikao cha kusikiza kesi ya Uchaguzi wa Urais.

Kesi ya uchaguzi ni nini?

Kesi ya uchaguzi ni utaratibu rasmi wa kupinga mchakato au matokeo ya upinzani mkali wa uchaguzi mahakamani. Ni wasilisho katika mahakama ya uchaguzi linalopinga uhalali wa mchakato, matokeo au dhana nyingine yoyote ya uchaguzi. Linaweza kuwasilishwa na mgombezi au hata mtu yeyote ambaye angependa kupinga dhana yoyote ya mchakato wa uchaguzi.

Katika katiba ya Kenya ya 2010, vyeo vya uchaguzi vinaashiria uchaguzi ule wa kirais, kibunge, gavana (kigavana) au ule wa kaunti na vinajumuisha hata uchaguzi-mdogo.

Kesi ya uchaguzi si ubishi wa kawaida wa kisheria kati ya watu. Ingawaje huenda ikajumuisha wahusika wachache, inachukuliwa kama ugombezi ambapo matamanio na haki za wapigaji kura zinatiliwa maanani na yako mbali sana na sheria zinazotawala aina nyingine za ubishi wa kisheria, sheria spesheli ya utaratibu na uzito zinatumika katika kesi za uchaguzi.

Kesi za uchaguzi zinazopinga dhana yoyote ya uchaguzi wa rais zinasajiliwa na kusikizwa katika Mahakama ya Juu zaidi (Kipengee cha 163 (3) cha Katiba). Aidha, kesi za uchaguzi zinazopinga uchaguzi wa Bungeni na Kaunti husikizwa katika Mahakama Kuu (Kipengee cha 165 (3) (a) cha Katiba) na mahakama ya Hakimu ya Mkazi (Sehemu ya 75 ya Kifungu cha Sheria cha Uchaguzi) mtawalia.

Kuhusiana na wajibu wa kutoa ushahidi (wajibu wa kuthibitisha) na kiwango ambacho mlalamishi anahitajika kuthibitisha kesi yake (wastani wa kuthibitisha) Mahakama ya Juu zaidi katika kesi hii yalikariri kwamba sababu ya uchaguzi inaanzishwa vizuri kwa njia sawa na kesi ya kawaida kati ya watu (sababu ya kiraia) pale ambapo wajibu wa kisheria unabakia kwa mlalamishi, lakini, kutegemea na ubora wake wa kuwasilisha shughuli hii ya ushahidi, ushahidi wa kuthibitisha unaendelea kubadilika. Hatimaye, yote yanaishia kwenye mahakama ili yaweze kuamua kama kesi thabiti na isiyojibiwa imewasilishwa.

 

 

Kesi ya uchaguzi wa urais ni nini?

Kesi ya uchaguzi wa urais ni mchakato rasmi wa kupinga mchakato, matokeo au dhana yoyote ya uchaguzi wa Rais kulingana na Vipengee 136, 139 (1) (b) na 146 (2) (b) ya Katiba ya Kenya, 2010

 

 

Ni mahakama gani husikiza kesi ya uchaguzi wa urais?

Kwa mujibu wa Kipengee cha 163 (3) cha Katiba ya Kenya, 2010, mamlaka ya kisheria (mamlaka ya kusikiza na kuamua) kesi ya uchaguzi wa urais imo kwenye Mahakama ya Juu zaidi. Hali hii ya mamlaka ya kisheria ya Mahakama ya Juu zaidi ni jumlishi kumaanisha kwamba hakuna mahakama mengine yanayo mamlaka ya kusikia ubishi kama huu, na pia asilia, kumaanisha kwamba ubishi unaosajiliwa katika Mahakama ya Juu zaidi kwa mara ya kwanza kinyume cha mamlaka ya kisheria ya kukata rufaa pale ambapo Mahakama ya Juu zaidi husikiza ubishi kutokana na rufaa kutoka kwenye mahakama mengine.

 

 

Je, uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi katika kesi hii uliathiri uchaguzi wa wagombezi wa bungeni, ugavana na kaunti?

Katika uamuzi wake, Mahakama ya Juu zaidi ilijiepusha na maswala ambayo hayamo ndani ya mamlaka yake   – haswa maswala yanayohusiana na uchaguzi wa wabunge, gavana na  ule unaofanywa kwenye kaunti, kwani kwa mujibu wa sheria, hayo ni maswala ambayo  ni majukumu ya mahakama mengine. Basi kwa maoni ya Mahakama ya Juu, kwamba kutupiliwa mbali kwa uchaguzi wa urais kusingesababisha kubatilishwa kwa uchaguzi wote mkuu na kutupiliwa mbali kwa uchaguzi wa Urais hakufai kusababisha mgogoro wa  kikatiba, kwani mamlaka husika ya kutangaza uchaguzi wa rais kuwa batili yanatolewa na Katiba yenyewe.

Kwa wazo lilo hilo, Mahakama ilitaja kwamba katika kesi ya uchaguzi inahitajika kuonyesha madai mahsusi, yaliyo kwa muhtasari na yanayolenga mada husika na ambayo hailazimu kurefusha mamlaka ya Mahakama ya Juu zaidi ya mipaka yake iliyowekwa wazi kwenye katiba kwani Mahakama itaweza tu kutoa amri mahsusi zinazolenga uchaguzi wa urais.

 

 

Ni akina nani walihusika katika kesi hii ya uchaguzi wa urais?

Jumla ya kesi tatu za kupinga uchaguzi wa rais ziliweza kusajiliwa mahakamani na watu tofauti katika tarehe tofauti. Zote tatu ziliweza kuwekwa pamoja na kusikizwa kwa pamoja.

Wahusika wa kesi ya kwanza (kesi nambari 3/2013) walikuwa Bw. Moses Kiarie Kuria, Bw. Denis Njue Itumbi na Bi. Florence Jemimah Sergon ambao walikuwa ndio walalamishi na Bw. Ahmed Isaac Hassan, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wakiwa ndio washtakiwa.

Wahusika katika kesi ya pili (kesi nambari 4/2013) walikuwa Bi. Gladwell Wathoni Otieno na Bw. Zahid Rajan wakiwa ndio walalamishi na Bw. Isaac Hassan, Bw. Uhuru Kenyatta, Bw. William Ruto, hawa wakiwa ndio rais-mteuliwa na naibu rais-mteuliwa mtawalia, wakiwa ndio washtakiwa.

Wahusika wa kesi ya tatu (kesi nambari 5/2013) walikuwa Bw. Raila Amolo Odinga, mmojawapo wa wagombezi wa urais, akiwa ndiye mlalamishi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, Bw. Ahmed Isaac Hassan, Bw. Uhuru Muigai Kenyatta na Bw. William Samoei Ruto wakiwa ndio washtakiwa

Mahakama iliamua kesi hii ya tatu iwe ndiyo kesi ongozi/kuu.

 

 

Je, kesi ya uchaguzi wa urais ilikuwa tofauti vipi na kesi nyingine za awali za uchaguzi wa urais?

Kwanza, huu ndio ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza katika Katiba ya Kenya, 2010. Kwa mujibu wa hayo, kesi hii ya uchaguzi ilikuwa ya kipekee kwani iliweza kusajiliwa katika mfumo mpya wa utawala wa kikatiba na kisheria, na vilevile ndiyo iliyokuwa kesi ya kwanza ya uchaguzi kuweza kusajiliwa mahakamani, kusikizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Juu zaidi iliyoanzishwa katika katiba mpya.

Pili, huenda ndiyo ilikuwa kesi ya kwanza ya uchaguzi kusikizwa na kuamuliwa kwa ustahili wake. Kesi za awali zilizokuwa zinapinga uchaguzi wa rais zimekuwa kwa ujumla zikiamuliwa kwa misingi ya vikwazo vya sheria na utaratibu – kama vile kutoweza kuwasilisha mahakamani karatasi dhidi ya mshtakiwa kwa wakati unaofaa.

Awali, kesi zote za ubunge na urais ziliweza kusajiliwa kwenye Mahakama ya Juu zaidi na wahusika kupewa haki ya kukata rufaa katika Mahakama ya rufaa.

Tukiwa bado katika mawazo hayo, kuna kesi nyingine kama hii mbele ya Mahakama ya Juu zaidi nchini Ghana, ambapo mlalamishi anapinga uhalali na ukweli  wa uchaguzi uliofanywa mnamo Disemba 2012. Kesi hii ya Ghana iliyo mbele ya Mahakama ya Juu zaidi inazua maswala ambayo yamekuwa yakifanana pakubwa yakilinganishwa na ubishi huu nchini Kenya. Kule Ghana, chama cha New Patriotic Party (NPP) kiliweza kupinga ukweli na uwazi wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi yakipatia ushindi chama cha National Democratic Congress (NDC) na kuona kwamba mchakato wa uthibitishwaji wa matokeo na vyama vya kisiasa haukuwa wazi na kwamba tofauti kati ya jumla ya idadi ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa urais na ubunge.

 

 

Kwa nini kesi ya uchaguzi wa urais iliamuliwa ndani ya kipindi cha muda mfupi sana?

Kipengee 140 cha Katiba kilikariri kipimo hiki cha muda. Kipengee 140 (1) na (2) cha Katiba kinaweka wazi yafuatayo:

• Mtu yeyote anaweza kusajili Kesi katika Mahakama ya Juu zaidi ili kupinga uchaguzi wa Rais-mteuliwa ndani ya siku saba baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.

• Ndani ya siku kumi na nne baada ya kusajili kesi, katika kauli (1), Mahakama ya Juu zaidi itasikiza na kuamua kesi hiyo na uamuzi wake utakuwa wa mwisho.

Kwa mujibu wa toleo hili la Katiba, na kwa mujibu wa mamlaka yaliyowekewa mahakama na kipengee (163)(8) cha Katiba ambacho kilipatia mamlaka Mahakama ya Juu zaidi kuunda sheria za kuonyesha mamlaka yake; na kuzidisha msingi wa sehemu ya 31 kuhusiana na sheria za Kifungu cha sheria cha Mahakama ya Juu zaidi, Mahakama iliunda na kuchapisha Sheria za Mahakama ya Juu zaidi (Kesi ya Uchaguzi wa urais) 2013. Sheria hizi zilinuiwa kupatia nguvu ya utendakazi kipengee 140 cha Katiba.

Kama vile ambavyo Mahakama yenyewe ilitambua, kipindi kile cha siku 14 ambacho lazima Mahakama ingesikia na kuamua kesi hiyo ya uchaguzi kilifaa kuanza kuhesabiwa pindi tu mhusika yeyote angesajili kesi hiyo. Kipimo hiki cha muda kilikuwa cha kikatiba na kisingeweza kubadilishwa.

Katika sheria za Mahakama ya Juu zaidi (Kesi ya Uchaguzi wa urais) 2013, kifungu cha sheria cha 6, kesi inayopinga uchaguzi wa Rais-mteuliwa ilifaa kusajiliwa Mahakamani ndani ya siku saba baada ya tarehe ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.

Katika mojawapo ya uamuzi uliotolewa na Mahakama wakati kikao cha kesi hii kilipokuwa kikiendelea, Mahakama iliweza kuweka wazi yafuatayo kuwa malengo na vipimo vya muda vya kutiliwa maanani ndani ya kipindi hicho cha siku 14:

• Kesi ya uchaguzi wa urais kusajiliwa ndani ya siku saba baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais na Mahakama ya Juu zaidi kusikiza kesi hiyo ndani ya siku kumi na nne baada ya kusajiliwa kwa kesi hiyo. Siku kumi na nne zinaanza kuhesabiwa pindi tu baada ya kuasajiliwa kwa kesi hiyo.

• Mlalamishi anafaa kumwasilishia mshtakiwa habari hiyo ndani ya siku tatu baada ya kusajiliwa kwa kesi.

• Washtakiwa wanafaa kusajili majibu yao ndani ya siku tatu baada ya kusajiliwa kwa kesi.

• Kikao cha kabla ya kesi kuanza kusikizwa kitafanywa siku tisa baada ya kusajiliwa kwa kesi hiyo.

• Mahakama imepewa pia siku tatu kujizoesha na utetezi wa hoja kabla ya kuratibu kikao cha kabla ya kesi kuanza kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii lazima kufanyike ndani ya siku 14 za kusajiliwa kwa kesi hiyo.

Mahakama pia iliweza kuweka wazi kwamba huku mchakato wa uchaguzi ulikuwa umeishia katika kutangazwa kwa mshindi rais-mteuliwa asingeweza kuchukua mamlaka ofisini mwake mpaka kuamuliwa kwa kesi hii “Kule kurefushwa kwa kipindi cha rais-mteuliwa kuendelea kuwa mteuliwa, pamoja na rais anayestaafu kuendelea kushika hatamu ya uongozi, kungesababisha hali ya matarajio mengi na sintofahamu, vyote ambavyo visingekuwa bora kwa sababu ya masilahi ya umma. Uamuzi wa kipekee na haraka wa ubishi huu hivyo basi ulikuwa muhimu-kabisa”.

Kabla ya uamuzi wake wa mwisho, Mahakama ilitoa baadhi ya uamuzi. Uamuzi huu ulihusu nini?

Mahakama ilikuwa imetupilia mbali maombi mawili katika uamuzi uliofanywa kwenye vikao vya kabla ya kesi kuanza kusikizwa. Mojawapo ilikuwa ni amri ya kutoa stakabadhi fulani; nyingine ilihusu Arifa ya Kutoa rejista ya wapigaji kura iliyowekwa alama na iliyopatikana katika vituo chungu nzima vya kupigia kura kote nchini. Mahakama vilevile ilitoa amri ya kutojumuishwa katika taratibu zake cheti cha ziada cha kiapo kilichosajiliwa na Raila Odinga. Uamuzi wa Mahakama ulitokana na kutambua kwake kwamba cheti hicho cha kiapo cha ziada kilikuwa ni jaribio fiche la kuingiza mambo mapya hata baada ya muda wa kusajili kesi kupita, hali ambayo ingekuwa kinyume cha mchakato huo wa kujiandaa katika kusikia kesi hiyo ambao haikuwa na muda-mrefu na pia ilihitaji nidhamu ya kiwango cha juu kama ilivyohitajika kwenye katiba.

Kwa nini Mahakama ya Juu zaidi ilitoa uamuzi yake kwanza na kisha kutoa sababu za uamuzi huo kwenye tarehe ya baadaye?

Ni mazoea ya kawaida ya mahakama, haswa wakati inapoishughulikia maswala yanayohitaji uamuzi wa haraka, kutoa uamuzi wake, na kuhifadhi tarehe ya baadaye ambapo hekima iliyosababisha uamuzi huo itaelezewa.

Sheria za Mahakama ya Juu zaidi (Kesi za Uchaguzi wa urais), 2013 kifungu cha 23 kijifungu cha sheria cha (1) inaruhusu Mahakama ya Juu zaidi baada ya uamuzi wa kesi kufikia mwisho wa kikao kutoa uamuzi wake lakini kuhifadhi sababu zake za uamuzi huo hadi katika tarehe ya baadaye. Sheria ndogo (2) inakariri kwamba pale ambapo Mahakama inahifadhi sababu za uamuzi wake katika sheria-ndogo (1), Mahakama itatoa muhtasari wa uamuzi wake na kipindi kile ambacho itaweza kutoa sababu zake.

Baada ya kusikiza hoja kutoka pande zote, mahakama iliweza kutafakari kuhusu kesi hiyo na kufikia uamuzi wa pamoja katika maswala yote yaliyokuwa yametengwa kufikiwa uamuzi. Uamuzi huo wa pamoja wa Mahakama ulisomwa mbele ya mahakama na Dr. Willy Mutunga, Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya juu zaidi, mnamo tarehe 30 Machi 2013. Wakati huo, Jaji Mkuu alikariri kuwa uamuzi ulio na maelezo na sababu za uamuzi huo ungetolewa wiki mbili baadaye, na hii iliweza kufanywa mnamo Aprili16, 2013.

Jaji Mkuu alikariri kuwa uamuzi huo utapatikana kwa umma kwenye kijitabu kitakachochapishwa na National Council of Law Reporting huku nayo Judicial Training Institute itakisambaza kotekote katika midahalo ya umma.

Wajibu wa Mwanasheria Mkuu akiwa Amicus Curiae yani Rafiki wa Mahakama ulikuwa ni upi?

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) imeanzishwa kwenye kipengee 156(4) ambacho kilimweka AG kuwa mshauri mkuu wa Serikali na kumpa AG mamlaka ya kuwakilisha serikali ya kitaifa mahakamani au katika taratibu nyingine zozote za kisheria ambazo serikali ya kitaifa inahusika mbali na taratibu za kihalifu. Kipengee 156(5) kinampa AG mamlaka, kwa idhini ya mahakama, mamlaka ya kuwa Amicus Curiae hii ni istilahi ya kilatino inayomaanisha rafiki wa mahakama katika taratibu zozote za kiraia ambazo Serikali haihusiki.

Hekima iliyosababisha kujiunga kwa Mwanasheria Mkuu katika kesi hiyo akiwa amicus curiae yani rafiki wa mahakama iliwekwa wazi na Mahakama ya Juu zaidi ifuatavyo:

•  Akiwa ndiye Ofisa Mkuu wa Ofisi ya Sheria ya Serikali lazima awe ndiye mwangalizi wa nyenzo za kisheria za Awamu ya Watoaji Uamuzi wa Serikali na mshauri anayetambuliwa na serikali katika masuala ya maslahi ya umma.

• Ofisi yake ndiyo ilikuwa ofisi kuu katika utendaji wa wajibu wa Watoaji Uamuzi ukilinganishwa na utekelezaji wa Katiba.

•  Katiba ilikuwa imeweka waziwazi kwamba katika hali fulani, Mwanasheria Mkuu huenda akapata kibali cha mahakama kuwepo akiwa amicus curiae.

• Mahakama ambayo ilikuwa muangalizi ya sheria za uhalali, nidhamu na kutopendelea kwenye Katiba na sheria yalibakia yameshika usukani katika kudhibiti wajibu maalum kama huo wa Mwanasheria Mkuu ambao angetekeleza endapo angekubaliwa kuwa amicus curiae.

• Kumkubali Mwanasheria Mkuu kuchukua wajibu huu kusingewasilisha mapendeleo yoyote ama mtazamo wa mamlaka ya mahakama ama kwa masilahi bora zaidi ya wahusika.

• Isingefaa kutojumuisha Mwanasheria Mkuu katika wajibu wa amicus curiae kwenye kesi hiyo.

Kwa nini taratibu za mahakamani ziliweza kurushwa moja kwa moja kwenye televisheni, tofauti na kesi za awali au kesi nyingine?

Isipokuwa zile taratibu ambazo zinahitajika na sheria kufanywa kwa vizuizi fulani kwa umma, kama vile taratibu zinazohusisha watoto, ni sheria na mazoea kufanya taratibu zote za mahakamani hadharani. Hata hivyo mahakama imewezeshwa kutekeleza vizuizi fulani kwa ufikivu wa umma na vyombo vya habari katika taratibu hizo ili kuhakikisha kila kitu kiko salama, usalama upo na utendakazi wa mpangilio katika shughuli za mahakamani unaendelea.

Kule kurushwa hewani kwa moja kwa moja kwa mara ya kwanza kwa kesi hii ya uchaguzi kulitosheleza maslahi mengi ya umma katika taratibu hizo na pia kukaweka kiwango kipya katika uwazi na unyofu wa vikao vya shirika hili la juu zaidi la mahakamani nchini.

Masuala makuu yaliyoibuliwa katika kesi yalikuwa yapi?

Kesi ya kwanza ilitetea kujumuishwa kwa kura zilizokataliwa kwenye hesabu ya mwisho ambayo, ilidaiwa, ilileta athari isiyofaa katika asilimia ya kura zilizopatikana kwa kila mgombezi.

Kesi ya pili ilipinga namna ambavyo mchakato wa uchaguzi ulifanywa na IEBC, kuhusiana na uchaguzi wa urais. Kwa ujumla, ilidaiwa kwamba uchaguzi huu ulifanywa kulingana na Katiba, Kifungu cha Uchaguzi, 2011 na taratibu zake Tumizi.

Kesi ya tatu ilipinga vikali uhalali wa kutangazwa kwa Uhuru Kenyatta na William Ruto kuwa Rais-mteuliwa na Naibu wa Rais-mteuliwa mtawalia na IEBC.

Katika kesi ile iliyofungamanishwa pamoja ilidaiwa kwamba mchakato wa uchaguzi ulikuwa na makosa chungu nzima kiasi cha kwamba ilikuwa haiwezekani kutambua kama matokeo ya urais yaliyotangazwa yalikuwa ya kihalali.

Nani ndiye aliye na wajibu wa kutoa ushahidi na hadi kiwango kipi ndipo mlalamishi anahitajika kuthibitisha kesi yake?

Katika sheria, wajibu wa kutoa ushahidi unajulikana kama wajibu wa kuthibitisha, nacho kiwango ambacho madai hayo yanahitajika kuthibitishwa kinaitwa wastani wa kuthibitisha.

Kanuni za kawaida za sheria ni kwamba katika kesi za kihalifu, isipokuwa tu katika kesi fulani zilizofafanuliwa-vizuri, wajibu wa kuthibitisha huwa kwenye upande wa mashtaka, nayo wastani wa kuthibitisha ni thibitisho linalozidi hali yoyote ya kutoeleweka. Katika kesi za kawaida kati ya watu binafsi au mashirika (kesi ya madai) wajibu wa kuthibitisha kwa kawaida huwa kwa yule mtu ambaye anasajili madai nayo wastani wa kuthibitisha ni thibitisho katika usawazisho wa uwezekano. Thibitisho katika usawazisho wa uwezekano huchukuliwa kuwa kwa ulinganishi dhaifu zaidi katika kiwango kile ambacho ushahidi huo unaeleweka zaidi ya kutoushuku.

Katika kesi hii, Mahakama ya Juu zaidi iliweza kuchukulia hali spesheli ya kesi ya uchaguzi na kutoa maoni yafuatayo kuhusu ule wajibu wa kuthibitisha na wastani wa kuthibitisha katika namna zifuatazo:

•    Kesi ya uchaguzi inapatikana kwa njia ileile kama ile ya kiraia pale ambapo ule wajibu wa kuthibitisha kisheria unakuwa kwa mujibu wake mlalamishi, lakini, kutegemea na ubora ambao yeye anauwasilisha, ule ushahidi wa kuthibitisha huendelea kubadilika. Hatimaye, bila shaka, huishia kwa Mahakama kuamua kama kesi thabiti na isiyojibiwa imeweza kuwasilishwa.

•    Kwa jumla, ni jukumu la mlalamishi kuwasilisha ushahidi wenye kuaminika na mahakama au ushahidi ulio na ushawishi mkubwa. Hata hivyo, kiwango cha ushawishi wa ushahidi unaotolewa katika kesi za aina hii kimepita kiwango kinachozingatiwa katika kesi nyingine za kibinafsi, ilhali ni chini ya kiwango kinachozingatiwa katika kesi za uhalifu au mashtaka. Katika kesi ya mahitaji ya data-mahsusi katika uchaguzi (kama vile kile kiwango kilichowekwa wazi katika Kipengee cha 138(4) cha Katiba, kwa ushindi wa kipekee kwenye uchaguzi wa urais, mhusika aliye na wajibu wa kisheria lazima ajiwasilishe hadi kufikia kiwango kisichofikiriwa wala kushukiwa.

•    Kunao mtazamo wa sheria maarufu ambao umekuwepo kwa mujibu wa mambo yasiyofuata kanuni na yanayodaiwa kwenye vifungu vya sheria vya mashirika ya umma kwamba vifungu vyote vya sheria vinachukuliwa kuwa vilifanywa kwa usahihi na kwa uzoefu. Pale ambapo mtu anadai kuto-fuata sheria ya uchaguzi, mlalamishi hafai tu kuthibitisha kwamba kumekuwepo na kuto-fuatwa kwa sheria, lakini kwamba kushindikana kama huko kwa ukubalifu kuliathiri usahihi wa uchaguzi, ni katika msingi huo ambao mshtakiwa anakuwa na wajibu wa kuthibitisha kinyume cha hayo. Kwa hivyo, mlalamishi lazima aweke wazi kauli ya kuwasilisha ushahidi thabiti na sahihi ya kule kutoka katika mamlaka ya umma ukirejelea ule ushauri wa sheria.

Mojawapo ya maswala nyeti katika uchaguzi ilikuwa ni kubainisha kama katika kupiga hesabu ya jumla ya kura zilizopigwa, IEBC ilifaa kujumuisha ‘kura zilizokataliwa’. Je Mahakama iliamua vipi kuhusu swala hili?

Kwa hakika, hili lilikuwa mojawapo la swala nyeti na katika kutoa uamuzi wake Mahakama iliangalia maneno ya katiba, kifungu Cha Sheria ya Uchaguzi na taratibu zake pamoja na uamuzi wa Mahakama mengine, na kuweza kutaja yafuatayo:

Si katiba wala Kifungu cha Sheria cha Uchaguzi, 2011 vinafafanua kauli “kura zilizoharibika”. Taratibu za Uchaguzi (Mkuu), 2012, huku zikikariri kwamba “karatasi ya kupigia kura iliyoharibika”, na “kura zenye ubishi” havifafanui kauli ya “kura iliyokataliwa.”

Sehemu ya ufasiri ya Kifungu cha sheria cha Uchaguzi inakariri kwamba  ‘karatasi ya kupigia kura’’ “inamaanisha karatasi inayotumiwa kurekodi chaguo lililofanywa na mpigaji kura na litajumuisha hata toleo la elektroniki la karatasi hiyo ya kupigia kura au kitu kingine kama hicho kwa makusudio ya kupigia kura kwa njia ya kieletroniki.”

Wakati kauli ‘karatasi ya kupigia kura iliyokataliwa’ inachukuliwa pamoja na kauli ‘karatasi ya kupigia kura iliyoharibika’ basi kwa mujibu wa taratibu ya 71 ya Taratibu za Uchaguzi (Mkuu), 2012 basi hii itakuwa ni karatasi ya kupigia kura ambayo ilikuwa imeshughulikiwa na mpigaji kura kwa njia ambayo haiwezi kutumiwa inavyofaa kama karatasi ya kupigia kura. Utaratibu unakariri kwamba karatasi kama hiyo ya kupigia kura lazima iachwe kwa yule ofisa msimamizi na nyingine kutolewa badala yake, na karatasi ile iliyoharibika kutupwa. Kwa hivyo ilikuwa wazi kwamba katika sheria, ‘karatasi ya kura iliyoharibika’ haitahesabiwa katika lile debe la kupigia kura na hivyo basi haichukuliwi kama kura.

Nchi tofauti hurejelea kura zilizopigwa kwa kauli tofauti, na kupatia athari zinazotofautiana katika kategoria za kura hizo zinazokinzana. Nchini Ghana, Cyprus na Portugal, mshindi wa uchaguzi anapatikana tu kutokana na kura halali zilizopigwa. Katika Katiba ya Ushelisheli, kauli pana “kura zilizopigwa” sawa tu na nchini Kenya, imeweza kuchukuliwa na kutumiwa. Mfano mkuu kuliko wote unaojitenga kutoka katika fikra hizi za mawazo ni katika Katiba ya Croatia ambayo inakariri kwamba “Rais atateuliwa na wingi wa wapigaji kura wote waliopiga kura” hivyo basi katika kuhesabiwa kwa kura, kura batili kunatiliwa maanani.

Taratibu zilzowekwa na IEBC hazitaji na kuzungumzia ya “kura zilizokataliwa” ingawaje zinatoa nafasi ya “karatasi za kupiga kura zilizokataliwa”, “karatasi za kupiga kura zilizoharibika”, na “kura zilizo na ubishi”. Ni wazi kwamba “karatasi za kupiga kura zilizoharibika” ni zile ambazo hazitumbukizwi kwenye debe la kupigia kura, lakini zinatupiliwa mbali na kubadilishwa pale zinapohitajika, na ofisa msimamizi katika kituo cha kupigia kura.

Hii inatofautiana na “karatasi za kupigia kura zilizokataliwa” ambazo, ingawaje zinawekwa kwenye debe-la kupigia kura, huwa zinatangazwa batili, kwa msingi wa mambo fulani yaliyobainishwa kwenye taratibu za uchaguzi – kama vile ulaghai, kuweka alama mara mbili, na upungufu mwingine kama huo.

Hakuna sheria na Taratibu inayoleta utofauti kati ya “kura” na “karatasi ya kupigia kura”,  hata ingawaje kwenye Kifungu cha sheria cha Uchaguzi na taratibu zake wote wametumia kauli hizi kumaanisha maana moja.

Kutokana na haya, mahakama iliweza kufikia katika hitimisho kwamba si bunge, wala IEBC walikuwa wameambatanisha umuhimu wowote katika uwezekano wa maana tofauti; hali ambayo ilisababisha Mahakama kuhitimisha kwamba karatasi ya kupigia kura iliyowekwa alama na kutumbukizwa kwenye debe la upigaji kura, imekuwa ikitazamiwa kwa siku zote kuwa kura; hivyo basi, karatasi ya upigaji kura iliyowekwa alama na kutumbukizwa kwenye debe la upigaji kura inaweza kuwa kura halali au kura iliyokataliwa.

Kwa sababu, kikanuni, karatasi ya kupigia kura iliyowekwa alama vizuri, au kura yenyewe, huhesabiwa na kuwa na nguvu kwa yule mgombezi aliyenuiwa, basi hiyo ndiyo kura halali; lakini karatasi ile ya kupigia kura isiyo – kubalifu, au kura, haitahesabiwa kwenye hesabu za mgombezi yeyote; haitakataliwa tu lakini pia inakuwa batili, na haileti mapendeleo yoyote ya uchaguzi kwa mgombezi yeyote. Kwa hali hiyo, kura iliyokataliwa haifai.

Kufikia hapa, Mahakama ilijiuliza swali muhimu-sana: kwa nini kura kama hii, au karatasi ya kupigia kura ambayo haiwezi kumpatia mgombezi yeyote mapendeleo ya kitarakimu, ifanywe kuwa ndiyo msingi wa kupiga hesabu ya asilimia ya kujumlishwa kwa kura ili kuweza kuthibitisha kwamba mgombezi mmoja au mwengine aliweza kufikia kiwango kile cha 50% +1 – na hivyo basi mgombezi kama huyo kutangazwa kuwa mshindi kamilifu wa uchaguzi wa urais, na hivyo basi kusiwe tena na uchaguzi mwingine wa kurudiwa?

Katika kulijibu swali hili Mahakama ilifikia katika ufasiri wa kauli ‘kura zilizopigwa’ katika Kipengee cha 138(4) cha Katiba kwa kurejelea tu kura halali zilizopigwa, na si kujumuisha karatasi za upigaji kura au kura zilizopigwa ambazo baadaye zinakataliwa kwa kutokuwa kubalifu na sheria. Mahakama iliweza kufikia katika ufasiri huu baada ya kutilia maanani:

• Mamlaka ya mahakama katika kufasiri Katiba kwa njia ambayo ‘itachangia katika utawala bora’ [Kipengee 259(1)(d)”]

• Wajibu wa kufasiri Katiba kwa njia ambayo inastawisha makusudio na kanuni zake, inapigisha hatua kanuni ya sheria na Sheria ya Haki za Binadamu pamoja na kuruhusu maendeleo ya sheria [kipengee 259]; na sifa bainishi na endelevu ya Katiba.

Mahakama iligundua nini kuhusu kuhesabiwa kwa kura?

Mahakama iligundua kwamba kuhesabiwa kwa kura katika Kituo cha Kitaifa cha Kuhesabu Kura kulifanywa kulingana na sheria, na kule kuhamishwa kwa wakala wa vyama vya kisiasa hakukudhoofisha ukweli wa hesabu hizo, wala kuleta msingi mzuri wa kutupilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais. Mahakama iligundua kwamba hakukuwa na ushahidi wowote wa kuunga mkono madai hayo ya uchezeaji na ukiukaji wa sheria kwenye upande wa IEBC katika swala la kuhesabu kura.

Uamuzi wa Mahakama kuhusiana na usahihi na ukweli wa rejista ya wapigaji kura ulikuwa upi?

Katika swala hili, Mahakama iliweza kuweka wazi kwamba lazima ingekuwa makinifu katika kuepuka kutoa amri ambayo ingeleta mgogoro kati ya mamlaka yake ya kisheria na yale ya mahakama zingine kama vile Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu ambazo zilikuwa na mamlaka ya kisheria ya kusikiliza mizozo ya uchaguzi wa vyeo vingine mbali na vile vya urais, vyote ambavyo vilitumia rejista hiyo moja ya wapigaji kura. Mahakama ya Juu zaidi hivyo basi ingeweza tu kuchunguza madai yoyote ya mwenendo mbaya wa  usajili wa wapigaji kura, pale ambapo ilidaiwa kwamba ziliathiri uhalali wa uchaguzi wa urais.

Hatimaye, Mahakama iligundua kwamba Rejista Kuu ya Wapigaji kura ndiyo iliyotumika pekee. Rejista Kuu ni mseto wa sehemu mbalimbali zilizotayarishwa katika kutosheleza makundi mbalimbali ya wapigaji kura. Hata hivyo, Rejista Kuu ya wapigaji kura inayo sehemu tatu ambazo ni; Rejista ya Wapigaji kura wa Bayometriki, Rejista spesheli na kitabu kijulikanacho kwa jina Green book, ambacho pia kinafahamika kuwa Kitabu Msingi cha Marejeleo, ambacho kinatumiwa kwa mkono.

Mahakama haikupata mambo mengi yasiyo ya kawaida kati ya idadi ya wapigaji kura waliosajiliwa na idadi ya jumla katika matokeo ya uchaguzi wa urais uliotangazwa na IEBC. Mambo yasiyo kawaida yaliyogunduliwa hayakuwa mengi kiasi cha kuathiri ukweli wa mchakato wa uchaguzi, na mbali na hayo, hakuna ushahidi wa ukweli uliopatikana wa kuonyesha kwamba mambo yasiyofuata kanuni kama hayo yalipangwa awali na kuingizwa na IEBC kwa manufaa ya kusababisha udhalalishwaji wa mgombezi yeyote maalum.

Mahakama ilihitimisha kwamba mchakato wa usajili wa wapigaji kura, kwa ujumla, ulikuwa wazi, sahihi, na wa kuthibitishwa; na kwamba rejista ya wapigaji kura iliyosanywa kutoka kwenye mchakato huu ilitumika katika kuwezesha kufanywa kwa uchaguzi huru, usiopendelea na wazi.

Rejista Spesheli ya Wapigaji kura ni nini?

Rejista spesheli inaundwa kuweza kutumika kwa watu ambao sifa zao hazikuweza kuchukuliwa na mtambo ule wa Usajili wa Wapigaji kura wa Bayometriki (BVR) hususan, imeundiwa watu walio na ulemavu. Rejista hii spesheli inalenga katika kuhakikisha kwamba raia wa uwezo wote wanajumuishwa katika rejista hiyo.

Mahakama iligundua nini kuhusiana na matumizi ya mfumo wa elektroniki wa kuhesabu na kuonyeshwa kwa matokeo na IEBC pamoja na uamuzi wake wa baadaye wa kurudi katika mfumo wa kuhesabu kura bila mitambo?

Mahakama ilitaja kwamba IEBC ilistahili kurudi katika matumizi ya mfumo wa kuhesabu bila mitambo kwani katiba na sheria za uchaguzi ziliipa IEBC haswa uhuru wa kufanya kazi katika mfumo kamilifu wa elektroniki au mfumo usio wa mitambo. Mahakama ilitambua kwamba kutokana na upungufu mkuu wa mifumo ya elektroniki na hoja kwamba mfumo wa kutotumia mitambo haukuwa umetajwa kuwa na makosa, hesabu hizo zisingeweza kupingwa. Mahakama iliweka wazi kwamba baada ya kushindikana kwa mfumo wa kuonyesha matokeo kwa njia ya elektroniki, hakukuwa na njia nyingine kwa IEBC ila kurudi katika mfumo wa uchaguzi usiotumia mitambo.

Mahakama ilisema nini kuhusu ununuzi wa huduma za teknolojia na IEBC?

Mahakama ilijali sana hali hiyo ya kushindikana kwa teknolojia hizo mbili, kwa jina Utambulisho wa Wapigaji kura kwa njia ya Elektroniki (EVID) na Mfumo wa Kuonyesha Matokeo (RTS), huenda kulitokana na “kutoelewana na mivutano miongoni mwa wanachama wa IEBC katika wakati wa mchakato wa ununuzi – mivutano ambayo iliwasababisha kutoweza kutathmini usahihi wa teknolojia hizi kabla ya wakati”. Mahakama iliweka wazi zaidi kwamba “huenda” mchakato huu wa kutumia teknolojia hizi “ulijawa na watu kushindana kupata masilahi yao na wengine kuwa na utovu wa nidhamu, au hata uhalifu” na ikapendekeza kwamba swala hili liachiwe wakala wa Serikali wanaohusika, kwa uchunguzi zaidi na kufunguliwa mashtaka kwa washukiwa ikiwezekana.

Uamuzi wa mwisho wa mahakama ulikuwa upi?

Kwa misingi ya hayo yaliyopatikana mahakama iliamua kwamba:
●  Uhuru Kenyatta na William Ruto walikuwa wameteuliwa na kutangazwa kihalali kuwa Rais-mteuliwa na Naibu Rais-Mteuliwa mtawalia;

● Uchaguzi wa urais ulikuwa umefanywa kwa njia huru, bila mapendeleo, kwa unyofu na ukweli katika kufuata katiba na sheria;

● Kura zilizokataliwa hazikufaa kujumuishwa katika kupiga hesabu ya mwisho   na kuchangia kwenye jumla ya hesabu kura ya kila mgombezi wa urais;

● Mahakama haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kutangaza kupigwe     hesabu upya kwa asilimia na mwenyekiti wa IEBC;

● Kila mhusika aliyehusika kwenye kesi ya uchaguzi angegharimia gharama zake mwenyewe.

Nini kingefanyika kama mahakama ingepata kwamba uchaguzi wa urais ulikuwa batili?

Kwa hakika , Mahakama ya Juu zaidi ingekuwa na nafasi ya kutoa maoni yake katika swala hili, kutokana na swali lililoulizwa na Mwanasheria-Mkuu: “Je uchaguzi mpya uliotazamiwa katika Kipengee 140(3) cha Katiba ulimaanisha uchaguzi wote wa urais (ukiwemo mchakato wa uteuzi)”, au  [u]namaanisha uchaguzi sawa na huo kama ulivyotazamiwa katika kipengee cha 138(5) na (7) – ukiwa na wagombezi walewale waliokuwa katika uchaguzi wa awali?

Kuhusu hili, Mahakama iliweza kuweka wazi yafuatayo:
• Ni wazi kwamba uchaguzi mpya katika Kipengee 140(3) unajitokeza kutokana na kubatilishwa kwa uchaguzi wa Rais-mteuliwa aliyetangazwa, na Mahakama ya Juu zaidi, kutokana na kesi iliyofanikiwa dhidi ya uchaguzi  kama huu. Kwa sababu uchaguzi mpya kama huu ni kwa mujibu wa uchaguzi kuweza kubatilishwa, basi unaweza tu kuhusisha wagombezi waliohusika katika uchaguzi wa mwanzo. Katika hali kama hiyo, hakutakuwa na msingi wowote wa uteuzi mpya wa wagombezi wa uchaguzi wowote kwa ugombezi huo utakaotokea.

• Hata hivyo, pale ambapo wagombezi, au mgombezi ambaye alishiriki katika uchaguzi wa mwanzo anakufa au anatupilia mbali ugombezi huo wa uchaguzi kabla ya tarehe iliyopangwa ya kufanyika kwa uchaguzi huo: basi toleo za Kipengee 138(1)(b) zitaweza kutumika na uteuzi mpya utafuata.

• Jibu la swali kuhusu “uchaguzi mpya” ambalo limefikiriwa katika Kipengee 140(3) lina maana sawa kama lile lililofikiriwa katika Kipengee 138(5) na (7) kutegemea na hali ya kesi hiyo ambayo ilibatilisha uchaguzi wa mwanzo. Kama mlalamishi angekuwa tu mmoja wa wagombezi, na ambaye aliibuka kuwa nafasi ya pili katika jumla ya hesabu ya kura baada ya Rais-mteuliwa, basi “uchaguzi mpya”, utaweza, katika sheria, kufanywa kati ya huyo mlalamishi na Rais-mteuliwa. Wagombezi wote wanaobakia ambao hawakugombea katika uchaguzi huo wa Rais-mteuliwa watachukuliwa kwamba walikubali kushindwa ama waliyakubali matokeo yaliyotangazwa na IEBC; na wagombezi kama hao huenda wasishiriki katika “uchaguzi mpya.”

• Kama ilivyokuwa hali katika kesi hii, kama mahakama ingeweza kubatilisha uchaguzi wa Uhuru Kenyatta na William Ruto, basi Raila Odinga angeshiriki kama mgombezi katika ‘uchaguzi mpya’ dhidi ya Rais-mteuliwa na yule mgombezi ambaye angepata kura nyingi zaidi angetangazwa kuwa Rais.

• Katika hali ambayo kesi inayopinga Rais-mteuliwa itasajiliwa na zaidi ya mgombezi mmoja ambao walishiriki katika uchaguzi wa kwanza nayo kesi hiyo ikafanikiwa, wagombezi watakaokuwa katika uchaguzi mpya watakuwa wale walalamishi pamoja na Rais-mteuliwa aliyetangazwa ambaye uchaguzi wake ulikuwa umekataliwa.

• Katika hali ambapo uchaguzi wa Rais-mteuliwa aliyetangazwa unakataliwa kutokana na kesi iliyowasilishwa na mtu ambaye hakuwa mgombezi katika uchaguzi wa mwanzo, basi wagombezi wote katika Uchaguzi wa urais wa mwanzo wataruhusiwa kushiriki katika “uchaguzi mpya”- na hakuna uteuzi mpya utahitajika.

www.kenyalaw.org – Pale ambapo taarifa ya kisheria ni maarifa ya umma
© – National Council for Law Reporting

Write a comment:

You must be logged in to post a comment.

© 2022 National Council for Law Reporting (Kenya Law) is ISO 9001:2015 Certified | Creative Commons | Privacy Policy & Disclaimer