You are here:       
Kenya Law / Blog / Kenya Law News: Hotuba yake Mpasua Msonobari kwenye uzinduzi wa Jina, Nembo,Toleo Dijito la Gazeti rasmi la Serikali na Tovuti ya Kenya Law.

Hotuba yake Mpasua Msonobari kwenye uzinduzi wa Jina, Nembo,Toleo Dijito la Gazeti rasmi la Serikali na Tovuti ya Kenya Law.

Mpasua Msonobari, Founder and CEO Languages Africa delivering his speech during the External Launch

Mpasua Msonobari, Founder and CEO Languages Africa delivering his speech during the External Launch

Asante sana kwa fursa hii adimu na ya kipekee kama magoti ya nyoka ya kuweza kumwakilisha mwananchi wa kawaida kwenye hafla hii ya kipekee ya uzinduzi wa jina, nembo na toleo dijito la gazeti rasmi la serikali na tovuti ya Kenya Law (KL).

 

Kwanza kabisa kabla sijapiga hatua zaidi katika mawasiliano yangu nanyi ningependa kuwapa salamu kutoka kwa wananchi wenzangu Wakenya wanaokipenda Kiswahili. Wameniomba niweze kumnukuu Mtaalamu mmoja wa Kiswahili, Mkereketwa wa Masuala ya Kiafrika na Mwanamitandao wa Kiswahili anayeitwa Mpasua Msonobari. Yeye husema Kiswahili Kitukuzwe, Kisifukuzwe. Hivyo basi nikiwaambia Kiswahili Kitukuzwe nitaomba mnijibu Kisifukuzwe. Jamani Eeh, Kiswahili Kitukuzwe?……Swadakta! Asanteni.

 

Salamu zikishafikishwa hivyo, maana ninavyosema siku zote, salamu ni kama kalamu humnyimi mtu, ningependa kutoa shukrani teule kwa aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji yani CEO wa KL, Bwana Michael Murungi kwa kukipatia Kiswahili uzito unaofaa na unaostahili na kuhakikisha kuwa nyaraka/stakabadhi mbalimbali za shirika la KL zinatafsiriwa na kuwekwa kwa lugha ya Kiswahili. Natumai yule aliyepokezwa kazi hii, Ndugu Longet Kiprono Terer, atendelea kuipeperusha bendera hii ya Kiswahili katika shirika hili la KL. Licha ya kuhakikisha kuwa Mpango wa Mikakati wa KL yani Strategic Plan upo kwa Kiswahili, KL imehakikisha ya kwamba Muhtasari wa ule uamuzi wa uchaguzi wa kura ya Kirais ya Machi 4 unapatikana kwa Kiswahili na vilevile baadhi ya uamuzi wa kesi mbalimbali za miezi 6 mfululizo zapatikana kwa Kiswahili. Hongereni sana KL na Kundi lako lote la Washikadau.

 

Ndugu wapenzi, KL kwa ujumla imejifunga kibwebwe katika kuhakikisha kuwa taarifa ya kisheria inakuwa maarifa kwa umma bila malipo yoyote kupitia mtandaoni! Shime! Shime! Shime! Naambiwa kuwa ndio wa kwanza kufanya hivi barani Afrika na ni miongoni mwa wale wachache waliofanya hivyo kote ulimwenguni. Wafanyikazi wake wa Idara zake zote wamechangamka kidijito yani kidijitali wanavyosema watoto wa Nairobi na ni watendakazi maridhawa. Si Pascal Othieno katika Idara ya Fedha, Si Cornelius Wekesa Lupao na Nelson Tunoi katika Idara ya Kuripotia Sheria, Si Linda Awuor kwenye Idara ya Utafiti na Maendeleo, Si Martin Andago wa Idara ya Taarifa, Mawasiliano na Teknolojia yani ICT, Si Wambui Kamau wa Idara ya Sheria za Kenya, Si Janet Watila wa Idara ya Wafanyikazi na Masuala ya Utawala, Si Edna Kuria na Lydia Midecha wa Idara ya Mikakati, Uhakikisho wa Ubora na Usimamizi wa Utendakazi, Si Emily Nakhungu na Carolyne Wairimu wa Idara ya Uuzaji na Mawasiliano na wengine wote. Hongereni sana. Endelezeni bidii na wala msilegeze kamba katu mkaja kupasulia chungu langoni.

 

Ndugu Mutunga asante kwa kutunga maadili na uadilifu wa kipekee ukiwa ndiwe Rais wa Idara ya Mahakama na Jaji Mkuu. Nawe Ndugu Githu Muigai asante sana kwa werevu na ustadi wako wa Kisheria ukiwa ndiwe Mwanasheria Mkuu wa nchi yetu tukufu ya Kenya tangu mwaka wa 2011. Changamoto ninayowapa ni kuhakikisha kuwa katiba yetu tunayoienzi katika Kifungu kinachosema kuwa Lugha ya Kiswahili itakuwa lugha ya kitaifa na vilevile rasmi kinaweza kutekelezwa kikamilifu. Na nikisema kikamilifu, kwa niaba ya mwananchi wa kawaida, namaanisha kikamilifu Ndugu zangu na tena kwa wepesi mno. Naogopa kusema tu kwa haraka iwezekanavyo.

 

Maono na Ndoto yangu ni kuyaona maakaba yani archives yote ya uamuzi wa kesi zote zilizowahi kuamuliwa kwenye Idara ya Mahakama tangu Kenya kujinyakulia uhuru au hata kabla yakiwa pia kwa Kiswahili. Maono na Ndoto yangu ni kuyaona Maakaba yote ya Sheria za Kenya na machapisho ya Gazeti rasmi la serikali kama haya mnayoyazindua leo kwa lugha ya Kiingereza yakiwa pia kwa lugha ya Kiswahili. Maono na Ndoto yangu ni kuona siku moja mahakama yote kote nchini yakiwa na angaa wakalimani wawili wa Kiswahili ili kuwawezeshea wananchi kufurahia haki yao ya kikatiba ya kujieleza na kuelezewa taratibu za kesi yao kwa lugha ya Kiswahili endapo watapendelea hivyo.

 

Mshairi mmoja wa Kiafrika kwa jina Bwak anasema, na namnukuu kwa Kiingereza, “Every language has its soul and spirit.“ Tunafaa basi kuhakikisha ya kuwa nafsi na hali halisi ya lugha ya Kiswahili inashughulikiwa na kutiliwa maanani kutoka katika kila pembe ya nchi siku zote.

 

Mimi mwenyewe nimekuwa mkalimani wa Kiswahili kwa zaidi ya mwongo mmoja na nusu yani miaka kumi na mitano. Nakumbuka nilipokuwa nikikalimania yani Interpreting for Tume ya Haki Ukweli na Maridhiano yani TJRC nilivyohisi fahari na furaha moyoni mwangu kwa kusaidia kueleweka kikamilifu kwa taratibu hizo za mawasilisho ya mashahidi na maswali waliokuwa wakiulizwa na Makamishna wa Tume hiyo kwenye vikao mbalimbali walivyokuwa navyo kule Kaskazini Mashariki. Leo ninapoona kwenye skrini zote za kompyuta Google ikiwa kwa Kiswahili najivunia vilevile kwa kushirikishwa na kuwezesha Kiswahili kuingia kuko huko mtandaoni. Hivyo basi haya yote ninayowaelezea si ndoto tu za Alinacha au Abunwasi. Si Vitendawili tu ambavyo hatujui vitateguliwa lini wala Nyimbo za Udijito au Udijitali ambazo matokeo yake bado hatujaona. Ni, MAONO NA NDOTO, zinazowezekana. Anavyosema Guru Ustadh Wallah Bin Wallah siri sirini zipo za kuyawezesha maono na ndoto hizo nilizowatajia hivyo basi endapo swali lenu ni vipi mtakavyofikia ndoto na maono ya huyu Bwana Mswahili, Mpasua Msonobari msiwe na wasiwasi wala wahaka.

 

Katika kumalizia ningependa kuwaomba wakenya wote wanaonisikiliza; Walio ndani ya nchi na hata walio kule ughaibuni yani Diaspora, wakati umefika wetu sisi wakenya kuikumbatia vilivyo lugha yetu adhimu na adimu ya Kiswahili katika kila namna ya maana ya neno hilo kumbatia.

 

Kama tulivyotambua, ndio uzi ambao tunaweza kuutumia tu katika kusuka na kushonea fulana nzito ya uwiano, maridhiano na masikilizano katika msimu huu wa baridi kali ya ukabila na ukabaila. Napendekeza hoja hii ya kukitumia Kiswahili kwa njia inayostahili na kustahiki baina yetu kama njia mojawapo ya kupigana na ukabila na ukabaila hapa nchini kwetu. Naamini kuwa tukifanya hivi tutakuwa wastaarabu zaidi na kuanza kusonga mbali na kuwa washenzi kwani kama wanavyoimba kwenye nyimbo za taarabu hakuna kiumbe kitimilifu.

 

Wazazi nao wahimize watoto wao pia kukipenda Kiswahili na si kukipenda tu bali kukizungumza mara kwa mara. Enzi za kuogopa kufunza mtoto wako kukizungumza Kiswahili eti kwa sababu ataonekana maskini, mjinga au mshamba zimeisha na wala hazitarudi tena. Nani alisema kuwa Kiswahili ni umaskini, ujinga au ushamba? Mwongo huyo!!! Kiswahili kwa hakika kwa sasa ninavyozungumza ni kinyume cha hayo yote. Kiswahili ni utajiri, werevu na ni usasa na ustaarabu unaotibu ugonjwa wa ukabila na ugomvi baina yetu. Kama huamini nitazame na nisikilize kwa makini mimi Mpasua Msonobari ninayezungumza nanyi kwa sasa.

 

Mwisho ni kuirai na kuiomba serikali hii iliyo uongozini, ikiongozwa na Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta, kumbuka nami namwakilisha huyo mwananchi wa kawaida. Naam, nawarai na kuwaomba kuuendeleza huo udijito au udijitali wanavyoita watoto wa Nairobi hadi katika pia lugha ya Kiswahili. Uhakikishe kuwa wizara zote za serikali na hata kaunti zote 47 zimeobwa na ikibidi hata kuamrishwa kugeuza nyaraka/stakabadhi zao muhimu na wanazotumia katika utendakazi wa kila siku hadi katika lugha ya Kiswahili. Namaanisha nyaraka kama vile Tovuti zao yani websites, Mipango yao ya Mikakati yani Strategic Plans, Fomu za kujazwa na mwananchi wanayemhudumia, Mikataba ya Huduma yani Service Charters na kadhalika. Ukifanya hivyo basi watakuwa wanamfaa mwananchi wa kawaida kama vile KL walivyomfaa mwananchi wa kawaida kama mimi kwa kumfikishia taarifa ya kisheria kwake kwa lugha ya Kiswahili na tena bila ya malipo yoyote kupitia mtandaoni.

 

Kwa kumalizia kabisa, nawakumbusheni maneno ya Mahatma Gandhi aliyewahi kusema, na namnukuu kwa Kiingereza ‘In matters of conscience, the law of the majority has no place.’ Kwa hakika, ndani ya nafsi ya kila mmoja wetu, ile sauti ya dhamiri yani conscience ndiyo inayotuongoza na kutufaa siku zote. Mimi binafsi nadhani kuwa wakati umefika wa Wakenya kudadisi dhamiri yao wakitumia sheria ya nchi na wala si wingi wao. Hawawezi kufanya hivyo bila taarifa ya kisheria inayoelezea sheria hiyo ya nchi kwa kinagaubaga. Na hapo ndipo KL inapoingilia. KL inaufungua mlango wa Sheria za Kenya na kumwezesha kila raia wa Kenya kuingia kwenye nyumba ya Taarifa ya Kisheria na kupata kujisitiri vilivyo dhidi ya ujinga wa kutojua na kutoweza kujitetea. Hatimaye naomba nimrejelee vilevile Edmund Burke, mwanafilosofia wa Kiairishi wa karne ya kumi na nane aliyewahi kusema na namnukuu kwa Kiingereza, “Bad laws are the worst sort of tyranny.” Nitarudia kauli hiyo Wakenya Wenzangu, “…bad laws are the worst sort of tyranny.” Kwa hivyo ni jukumu letu sote kuzisoma, kuzitunga na kuzitekeleza sheria nzuri katika nchi yetu ili kuiepuka dhuluma hii.

 

KL, wametuanzishia vyema na kutuongoza kwa kukipatia Kiswahili hadhi na taadhima. Naomba sote tuweze kuwapigia makofi….. Hebu na tuwafuate unyo kwa unyo kwa kufanya vivyo hivyo popote pale tulipo. KL Hongereni sana kwa hatua hiyo mliyopiga katika lugha ya Kiswahili! Hongereni sana! Pongezi vilevile kwanza kwa uzinduzi wa Jina lenu na Nembo yenu, pili Toleo dijito la Gazeti Rasmi la Serikali ya Kenya na mwisho Tovuti yenu Iliyopandishwa Daraja na inayong’aa ajabu!

Asalaam Aleikum yani Amani ya Mwenyezi Mungu iwe nanyi.

 

Hotuba Imetayarishwa na Kuwasilishwa naye, Mpasua Msonobari, Mkereketwa & Mjasiriamali wa Lugha ya Kiswahili.

Write a comment:

You must be logged in to post a comment.

© 2022 National Council for Law Reporting (Kenya Law) is ISO 9001:2015 Certified | Creative Commons | Privacy Policy & Disclaimer